Shirika la Habari la Hawza - Kuhusiana wajibu na majukumu ya wanaosubiri, maneno mengi yamesemwa; lakini kwa ufupi inaweza kusemwa kwamba majukumu ya watu katika kipindi hiki yanagawanyika katika sehemu mbili:
Wajibu wa Kawaida
Wajibu huu, katika maneno ya Ma‘sūmīn (as), umetajwa miongoni mwa majukumu katika zama za ghaiba; lakini si mahsusi kwa kipindi hiki pekee, bali ni wajibu unaopasa kutekelezwa katika nyakati zote, huenda kutajwa kwake miongoni mwa wajibu katika zama za ghaiba ni kwa madhumuni ya kusisitiza tu.
Baadhi ya wajibu huu ni kama ifuatavyo:
1. Kumjua Imam wa Kila Zama
Miongoni mwa majukumu ambayo katika kila zama – hasa katika zama za ghaiba – yamesisitizwa na kuagizwa kwa wafuasi wa mafundisho ya Kiislamu ni kupatikana kwa maarifa na kumjua Imam wa zama hizo.
Imam as-Swādiq (as) amesema:
إِعْرِفْ إِمَامَکَ فَإِنَّکَ إِذَا عَرَفْتَ لَمْ یَضُرَّکَ تَقَدَّمَ هَذَا الْأَمْرُ أَوْ تَأَخَّرَ
Mjue Imam wako, kwa hakika ukimjua Imam wako, basi halitakudhuru jambo hili liwe limetangulia au limechelewa.
(al-Kāfī, juzuu 1, uk. 371)
Hakika kumjua Imam hakutengani na kumjua Mwenyezi Mungu Mtukufu; bali ni miongoni mwa vipengele vyake, kama ilivyo katika dua tukufu ya maarifa ambapo tunamuelekea Mwenyezi Mungu Mtukufu tukisema:
«اللَّهُمَّ عَرِّفْنِی نَفْسَکَ فَإِنَّکَ إِنْ لَمْ تُعَرِّفْنِی نَفْسَکَ لَمْ أَعْرِفْ نَبِیکَ اللَّهُمَّ عَرِّفْنِی رَسُولَکَ فَإِنَّکَ إِنْ لَمْ تُعَرِّفْنِی رَسُولَکَ لَمْ أَعْرِفْ حجّتکَ اللَّهُمَّ عَرِّفْنِی حجّتکَ فَإِنَّکَ إِنْ لَمْ تُعَرِّفْنِی حجّتکَ ضَلَلْتُ عَنْ دِینِی.»
Ewe Mwenyezi Mungu! Nijulishe nafsi yako, kwani ikiwa hutanijulisha nafsi yako, sitamjua Mtume wako. Ewe Mwenyezi Mungu! Nijulishe Mtume wako, kwani ikiwa hutanijulisha Mtume wako, sitamjua Hujja wako. Ewe Mwenyezi Mungu! Nijulishe Hujja wako, kwani ikiwa hutanijulisha Hujja wako, nitapotea kuepukana na dini yangu.
(al-Kāfī, juzuu 1, uk. 342)
Kutoka katika riwaya za Ma‘sūmīn (as) kwa uwazi tunapata kwamba fadhila zote na thamani zote za uja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu zinarejea katika kumfahamu Imam (as) na kushikamana nayo.
2. Kudumu katika Mapenzi ya Ahlul-Bayt (as).
Miongoni mwa majukumu muhimu katika kila zama ni kupenda na kuwapenda Ahlul-Bayt wa Mtume (saww) katika nafasi ya marafiki wa Mwenyezi Mungu, Katika zama za ghaiba ya mwisho ya Imamu Ma‘sūm, kwa sababu ya kuwa mafichoni Imamu, huenda mambo fulani yakamweka mtu mbali na jukumu hili muhimu, ndiyo maana katika riwaya imeagizwa kudumu juu ya mapenzi kwa nuru hizo tukufu.
Tusisahau kwamba mapenzi haya ni amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, miaka mingi kabla ya huyo Bwana kuanza maisha yake ya kidunia, watu safi walimuonesha mapenzi, Mtume Mtukufu s(aww), bora wa manabii na mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, alipokuwa akizungumza juu ya wasii wake wa mwisho, kwa heshima kubwa, alitumia maneno makubwa zaidi ya mapenzi, yaani: (بِأَبِی وَأُمِّی) Baba na mama yangu wawe fidia kwake, pale aliposema:
«بِأَبِی وَ أُمِّی سَمِیی وَشَبِیهِی وَشَبِیهُ مُوسَی بْنِ عِمْرَانَ عَلَیهِ جُیوبُ النُّور...»
Baba na mama yangu wawe fidia kwake! Kwani yeye ni jina langu, na mfano wangu, na mfano wa Musa bin Imran ambaye amezungukwa na nuru.
(Kifāyat al-Athar, uk. 156)
Na vilevile pale Ali bin Abi Ṭālib (as) alipokuwa akitazama zama za Imamu wa mwisho akasema:
«فَانْظُرُوا أَهْلَ بَیتِ نَبِیکُمْ فَإِنْ لَبَدُوا فَالْبُدُوا، وَ إِنِ اسْتَنْصَرُوکُمْ فَانْصُرُوهُمْ، فَلَیفَرِّجَنَّ اللَّهُ [الْفِتْنَةَ] بِرَجُلٍ مِنَّا أَهْلَ الْبَیتِ. بِأَبِی ابْنُ خِیرَةِ الْإِمَاءِ.»
Waangalieni Ahlul-Bayt wa Mtume wenu; ikiwa wamenyamaza na kukaa majumbani mwao, basi nanyi nyamazeni na shikamaneni na ardhi. Na wakikuombeni msaada, basi kimbilieni kuwanusuru. Hakika Mwenyezi Mungu atafungua [fitna] kwa mtu mmoja kutoka kwetu Ahlul-Bayt. Baba yangu awe fidia kwake! Yeye ni mwana wa mja bora wa kike.
(Bihār al-Anwār, juzuu 34, uk. 118)
Khalād bin Saffār anasema: Nilimuuliza Imam as-Swādiq (as): “Je, al-Qāim amezaliwa?”
Imam akasema:
«لَا وَ لَوْ أَدْرَکْتُهُ لَخَدَمْتُهُ أَیامَ حَیاتِی.»
La, na lau ningemdiriki, ningemtumikia katika siku za maisha yangu.
(Bihār al-Anwār, juzuu 51, uk. 148)
Katika riwaya nyingine pia Imam al-Bāqir (as) amesema:
«أَمَا إِنِّی لَوْ أَدْرَکْتُ ذَلِکَ لَأَبْقَیتُ نَفْسِی لِصَاحِبِ هَذَا الْأَمْر.»
Hakika, lau ningelifikia hilo, ningehifadhi nafsi yangu kwa ajili ya mwenye jambo hili.
(Bihār al-Anwār, juzuu 52, uk. 243)
Kwa kuzingatia riwaya zilizotajwa, hakuna shaka kwamba mapenzi ya Ahlul-Bayt (as) – hususan Hujja wa mwisho wa Mwenyezi Mungu – katika kipindi cha ghaiba ni jambo muhimu sana na lenye thamani kubwa.
3. Uchamungu na Kushikamana na Taqwa ya Mwenyezi Mungu
Taqwa ya Mwenyezi Mungu ni wajibu katika nyakati zote; lakini katika kipindi cha ghaiba, kutokana na hali zake maalum, umuhimu wake ni mkubwa zaidi. Hii ni kwa sababu katika kipindi hiki, kuna vichocheo vingi vinavyoshirikiana kumvuta mwanadamu katika njia isiyo sahihi na kumsababisha apotee.
Imam as-Swādiq (A.S.) amesema:
«إِنَّ لِصَاحِبِ هَذَا اَلْأَمْرِ غَیْبَةً فَلْیَتَّقِ اَللَّهَ عَبْدٌ وَ لْیَتَمَسَّکْ بِدِینِهِ.»
Hakika kwa mwenye jambo hili kuna ghaiba; basi mja na amche Mwenyezi Mungu na ashikamane na dini yake.
(Kamāl ad-Dīn, juzuu 2, uk. 343)
4. Kufuatilia Maagizo ya Maimamu (as)
Kwa kuwa maimamu wote (as) ni nuru moja, basi maagizo na maneno yao yote yanafuata lengo moja. Kwa hivyo, kumfuata mmoja wao ni sawa na kuwafuata wote. Katika wakati ambao mmoja wao hayupo wazi mbele ya watu, basi maagizo ya wengine hubaki kuwa taa ya uongofu.
Yūnus bin ‘Abdur-Raḥmān anasema: Niliingia kwa Mūsā bin Ja‘far (as) nikamwambia:
«یَا ابْنَ رَسُولِ اللَّهِ أَنْتَ الْقَائِمُ بِالْحَقِّ؟»
Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, wewe ndiye Qāim wa haki?
Akasema:
«أَنَا الْقَائِمُ بِالْحَقِّ وَ لَکِنَّ الْقَائِمَ الَّذِی یُطَهِّرُ الْأَرْضَ مِنْ أَعْدَاءِ اللَّهِ عَزَّ وَ جَلَّ وَ یَمْلَؤُهَا عَدْلًا کَمَا مُلِئَتْ جَوْراً وَ ظُلْماً هُوَ الْخَامِسُ مِنْ وُلْدِی لَهُ غَیْبَةٌ یَطُولُ أَمَدُهَا خَوْفاً عَلَی نَفْسِهِ یَرْتَدُّ فِیهَا أَقْوَامٌ وَ یَثْبُتُ فِیهَا آخَرُونَ ثُمَّ قَالَ (ع): طُوبَی لِشِیعَتِنَا الْمُتَمَسِّکِینَ بِحَبْلِنَا فِی غَیْبَةِ قَائِمِنَا الثَّابِتِینَ عَلَی مُوَالاتِنَا وَ الْبَرَاءَةِ مِنْ أَعْدَائِنَا أُولَئِکَ مِنَّا وَ نَحْنُ مِنْهُمْ قَدْ رَضُوا بِنَا أَئِمَّةً وَ رَضِینَا بِهِمْ شِیعَةً فَطُوبَی لَهُمْ ثُمَّ طُوبَی لَهُمْ وَ هُمْ وَ اللَّهِ مَعَنَا فِی دَرَجَاتِنَا یَوْمَ الْقِیَامَةِ.»
Mimi ndiye Qāim kwa haki, lakini Qāim ambaye atasafisha ardhi kutokana na maadui wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na ataijaza uadilifu kama ilivyojazwa dhulma na uonevu, huyo ni wa tano kati ya watoto wangu, atakuwa na ghaiba ya muda mrefu kwa sababu ya kuchelea nafsi yake. Katika ghaiba hiyo, baadhi ya watu watarudi nyuma na wengine watathibiti. Kisha akasema (as): Heri kwa Shia wetu wanaoshikamana na kamba yetu katika ghaiba ya Qāim wetu, walio thabiti katika mapenzi yetu na kujitenga na maadui zetu. Hao ni kutoka kwetu, na sisi ni kutoka kwao. Wameridhia sisi kuwa maimamu wao, nasi tumeridhia wao kuwa Shia wetu. Basi heri kwao, tena heri kwao, naapa kwa Mwenyezi Mungu, wao watakuwa pamoja nasi katika daraja zetu Siku ya Kiyama.
(Kamāl ad-Dīn wa Tamām an-Ni‘ma, juzuu 2, uk. 361)
Utafiti huu unaendelea …
Imenukuliwa kutoka kwenye kitabu kiitwacho: Darsnāmeh Mahdawiyyat kilichoandikwa na Khodā-Murād Salīmiyān, huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.
Maoni yako